Mamlaka ambayo inasimamia utabiri wa hali ya hewa nchini Tanzania imetangaza kwamba kimbunga Hidaya kilichoathiri pwani ya nchi hiyo kimefikia mwisho.
Taarifa ya mamlaka hiyo inaashiria kwamba kilifikia mwisho usiku wa manane Mei 4, 2024 kufuatia vipimo vilivyoonyesha kwamba kilipoteza kabisa nguvu zake na kuelekea nchi kavu kupitia kisiwa cha Mafia.
“Taarifa hii inahitimisha mfululizo wa taarifa za kilichokuwa Kimbunga “HIDAYA” zilizokuwa zikitolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) tangu tarehe 01 Mei 2024, mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa unaonyesha kuwa katika kipindi cha masaa 6 yaliyopita Kimbunga “HIDAYA” kimepoteza kabisa nguvu yake baada ya kuingia Nchi kavu katika kisiwa cha Mafia” ndiyo baadhi ya maneno kwenye taarifa hiyo rasmi.
TMA iliendelea kueleza kwamba mabaki ya mawingu ya mvua yaliyokuwa yameandamana na kimbunga hicho yalisambaa katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa kusini mwa Tanzania hasa mikoa ya Lindi, Mtwara, Morogoro na maeneo jirani.
Imehakikishia raia wa Tanzania kwamba hakuna tena tishio la kimbunga “HIDAYA” katika nchini humo.
Mvua ya masika hata hivyo inatarajiwa kuendelea katika baadhi ya maeneo kama karibu na ziwa Victoria, Nyanda za Juu kaskazini-mashariki na pwani ya kaskazini.
Kimbunga hicho Hidaya kilikuwa kimetabiriwa kufika katika Pwani ya Kenya ambapo serikali ilichukua hatua za tahadhari kama vile kupiga mafuruku shughuli zote za baharini.