Kimani Ichung’wah adai Raila Odinga anataka ‘Handshake’

Marion Bosire
2 Min Read

Kiongoozi wa walio wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah sasa anadai kwamba kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Coalition Raila Odinga anazua mtafaruku wa kisiasa ili kulazimisha serikali ya muungano almaarufu “Handshake”.

Kwenye taarifa Ichungwa alisema kwamba Odinga ana nia ya kuingia serikalini kupitia mlango wa nyuma kwa kusababisha ghasia na machafuko na hivyo kulemaza serikali ya sasa kupitia maandamano dhidi yake.

Kimani anahisi kwamba maandamano yanaongozwa na kukosa kwa upinzani kukubali ukweli na nia ya kutaka kuingia serikalini.

“Nia yao ni kukiuka sheria, muundo ni kusababisha machafuko na kuathiri biashara wakiwa na matumaini duni kwamba hilo litasababisha kuafikiwa kwa makubaliano ya kugawana mamlaka.” alisema Ichung’wah.

Kiongozi huyo alisema serikali inashughulikia suala la gharama ya juu ya maisha akidai kwamba maandamano yanayoshuhudiwa hayahusu gharama hiyo ya maisha bali ni fursa ya Raila kuonyesha kutoridhika kwake baada ya kushindwa kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Akizungumza kwa niaba ya serikali ya Kenya Kwanza Ichung’wah alimtaka inspekta mkuu wa polisi na mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa jinai kuchunguza visa vyote vya uhalifu vilivyotokea wakati wa maandamano, wakamate washukiwa na kuwafungulia mashtaka.

Anataka pia mkuu wa polisi achunguze madai ya kuundwa kwa magenge ya uhalifu ya kikabila ambayo huenda yakatumwa katika sehemu mbali mbali za nchi kuzua ghasia.

Website |  + posts
Share This Article