Majaji watatu wanaosikiliza kesi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua ya kupinga kutimuliwa kwake madarakani wataamua hii leo Ijumaa ikiwa wataendelea kusikiliza kesi hiyo au watajiondoa.
Hii ni baada ya Gachagua kuwataka kujiondoa kwa misingi kuwa wana uhusiano na upande wa utetezi kwenye kesi hiyo.
Wametoa mfano wa jinsi walivyoonyesha wazi kuwa na miegemeo katika uamuzi wao juu ya iwapo Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu alikuwa na mamlaka ya kuwateua kusikiliza kesi hiyo.
Jopo la majaji watatu ambao ni Eric Ogola, Anthony Mrima na Dkt. Freda Mugambi liliteuliwa na Mwilu Jumamosi wiki iliyopita kusikiliza kesi hiyo.
Hata hivyo, Gachagua, kupitia mawakili wake wakiongozwa na Paul Muite, anadai kuwa mkewe Jaji Ogola aliteuliwa na Rais William Ruto kwenye taasisi moja ya serikali na kwa misingi hiyo Jaji huyo ataupendelea upande wa utetezi.
Ruto ni mhusika kwenye kesi hiyo.
Jaji Mrima anadaiwa kuwa na uhusiano wa karibu na Spika wa Bunge la Seneti Jeffah Amason Kingi.
Ingawa Gachagua anataka majaji hao wote kujiondoa, hakumnyoshea kidole cha lawama Jaji Mugambi.
Upande wa utetezi ukiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa zamani Prof. Githu Muigai umepuuzilia mbali madai hayo ukiyataja kuwa yasiyokuwa na msingi.
Majaji hayo wanatarajiwa kutoa uamuzi wao kuhusu suala hilo leo Ijumaa, majira ya saa saba mchana.