Waziri wa elimu Julius Migos Ogamba, ameishukuru serikali ya Ujerumani kwa kusaidia sekta ya elimu hapa nchini Kupitia utoaji mafunzo na utafiti.
Kulingana na Ogamba, usaidizi huo umebuni mazingira Bora ya ubadilishanaji wa teknolojia, utamaduni na ujuzi.
Waziri huyo aliyasema hayo afisini mwake katika Jumba la Jogoo, alipokuwa mwenyeji wa balozi wa Ujerumani hapa nchini Sebastian Groth aliyemtembelea.
Katika mkutano huo, Waziri Ogamba alikuwa ameandamana na Katibu wa elimu ya msingi Dkt. Belio Kipsang, mwenzake wa mafunzo ya kiufundi (TVET), Dkt. Esther Muoria na Mkurugenzi wa elimu ya juu Darius Ogutu.
Kwa upande wake Dkt. Kipsang alisema jumla ya wanafunzi 10,000 wanafunzwa Lugha ya Kijerumani katika shule 130 za upili hapa nchini.
“Mpango wa kubadilishana wanafunzi kati ya shule za Kenya na Ujerumani umetoa fursa kwa wanafunzi hao kuimarisha uzungumzaji wa Kijerumani na kufurahia utamaduni wa Kijerumani,” alisema Kipsang’
Dkt. Muoria alisema ushirikiano huo umesaidia pakubwa taifa hili kunufaika na mafunzo ya kiufundi, ambao umekuwepo kwa Karne kadhaa.
“Ujerumani umetoa usaidizi wa kiufundi ambao umewawezesha wanafunzi kuwa tayari kwa soko la ajira punde wanapokamilisha masomo,” alisema Muoria.
Wakati wa mkutano huo, maafisa wa nchi hizo mbili walikubaliana kuimarisha ushirikiano, kwa manufaa ya raia WA nchi hizo.