Kenya inatambua umuhimu wa mchakato jumuishi wa amani nchini Sudan, ikisisitiza kuwa wahusika wote sharti washiriki meza ya mazungumzo ili kufanikisha mchakato huo.
Akizungumza alipokutana na Pekka Haavisto, Mjumbe wa kibinafsi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sudan, Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi, alitoa wito wa kupanuliwa kwa mchakato wa amani ili kuwajumuisha wazee, kina mama, vijana, jamii, viongozi wa dini na mashirika ya jamii, kuhakikisa uwakilishi mwafaka kwenye mchakato huo wa amani.
Aidha, Kenya ilisisitiza kuwa mzozo wa Sudan hauwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi, ikionya kuwa iwapo pande zote zitaendeleza utumizi wa jeshi, upatikanaji wa suluhu ya kudumu utadumazwa.
“Nilisisitiza kuwa amani haiwezi patikan kwa utumizi wa jeshi,” alisema Mudavadi.
Kenya ilitoa wito kwa pande zote kukumbatia mazungumzo ili kusitisha mzozo huo na kuokoa mamilioni ya maisha.
Wakati huo huo Mudavadi alielezea wasiwasi kuhusu kuendelea kuingizwa silaha nchini Sudan.