Kenya yalaani mashambulizi dhidi ya nchi nane Mashariki ya Kati

Nchi hiyo inatoa wito wa mazungumzo ya dharura yanayoleta pamoja washikadau mbalimbali ili kupunguza mzozo katika Mashariki ya Kati.

Martin Mwanje
2 Min Read
UAE ni miongoni mwa nchi zilizoshambuliwa na Iran / Picha kwa hisani ya Arab News

Kenya imelaani vikali mashambulizi dhidi ya nchi nane za Mashariki ya Kati katika mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati. 

Kwenye taarifa, Rais William Ruto amelaani mashambulizi dhidi ya nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu, (UAE), Qatar, Saudi Arabia, Iraq, Oman, Kuwait, Jordan na Bahrain.

“Ni ishara tosha kwamba mzozo huu wa kikanda ni tishio kubwa kwa amani na usalama duniani. Katika wakati huu muhimu na hatari katika historia ya dunia, taasisi za pande nyingi za muda mrefu zinasalia mipangokazi muhimu ya utatuzi wa janga la sasa katika Mashariki ya Kati,” alisema Rais Ruto.

“Kenya inatoa wito wa mazungumzo ya dharura yanayoleta pamoja washikadau mbalimbali ili kupunguza mzozo.”

Ruto alitoa wito wakati ambapo runinga ya taifa ya Iran imeripoti kwamba kiongozi mkuu wa nchi hiyo, Ayatollah Ali Khamenei, ameuawa.

Watu zaidi ya 200 pia wameripotiwa kuuawa katika mashambulizi yaliyotekelezwa na Marekani na Israel.

Marekani na Israel zilianzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran katika kile nchi hizo zinasema ni jitihada za kuizuia Iran kupata silaha za nyuklia.

Katika kujibu mashambulizi hayo, Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu cha Iran kinasema nchi hiyo nayo imeanzisha awamu yake ya kwanza ya mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel.

Nchini Marekani, wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walirushiana cheche kali za maneno kutokana na mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na nchi za Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Baraza hilo lilifanya mkutano wa dharura Jumamosi iliyopita.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, UN, Antonio Guterres akielezea mashaka kuhusu ongezeko zaidi la mapigano Mashariki ya Kati.

Guterres ametoa wito wa “kusitishwa mara moja kwa uhasama na kupunguza mzozo” kwa pande husika.

Share This Article