Rais William Ruto amekashifu jaribio la mauaji dhidi ya Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.
Kupitia mtandao wa X, kiongozi huyo wa taifa alitaja tukio hilo kuwa la kushtua na lisilokubalika.
“Kwa niaba ya raia na serikali ya Kenya, nakashifu jarabio la mauaji dhidi ya rais wa zamani wa Marekani Donald J. Trump,” alisema Rais Ruto.
Ruto alielezea huruma zake kwa Trump, familia yake na familia ya mshambulizi huyo.
“Namtakia Trump uponyaji wa haraka,” aliongeza Rais Ruto.
Trump alipigwa risasi kwenye sikio Jumamosi iliyopita, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara, anapojiandaa kwa uchaguzi wa urais mwezi Novemba mwaka huu.
Mshambulizi huyo wa Trump aliuawa na maafisa wa usalama wa Secret Service. Mtu mmoja alifariki na mwingine kujeruhiwa wakati wa shambulizi hilo.
Uchunguzi kuhusu kisa hicho unaendelea.