Kenya ilimaliza katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa medali ya makala ya 19 ya mashindano ya Riadha Duniani yaliyokamilika Jumapili usiku mjini Budapest, Hungary.
Kenya ilitwaa nishani 10, dhahabu 3, fedha 3 na shaba 4 yakiwa matokeo bora kuliko ya mwaka jana mjini Oregon nchini Marekani ilikozoa medali 10, dhahabu 2, fedha 5 na shaba 3.
Washindi wa medali katika makala ya mwaka huu kwa Kenya walikuwa: Faith Kipyegon aliyenyakua dhahabu katika mita 1,500 na mita 5,000 huku fedha zikitwaliwa na Emmanuel Wanyonyi katika mita 800, Daniel Simiu katika mita 10,000 na Beatrice Chepkoech katika mita 3,000 kuruka viunzi na maji.
Nishani nne za shaba za Kenya zilipatikana kupitia kwa Jacob Krop mita 5,000, Abraham Kibiwott mita 3,000 kuruka viunzi na maji, Beatrice Chebet mita 5,000 na Faith Cherotich mita 3,000 kuruka viunzi na maji.
Wanaume wanne na wanawake watano ndio walioishindia Kenya nishani katika mashindano hayo ya siku 9.
Kenya iliwakilishwa na jumla ya wanariadha 75.