Kampuni ya umeme ya Kenya Power inawahamasisha wateja wake milioni 9.2 kutumia umeme kupika maarfuku kama e-cooking.
Lengo ni kuongeza idadi ya wateja wanaotumia umeme kupika kutoka ile ya sasa ya wateja wapatao 90,000 hadi zaidi ya wateja 500,000 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Mkurugenzi Mkuu wa Kenya Power Mhandisi Joseph Siror alidokeza hilo alipozindua mpango unaohamasisha matumizi ya umeme katika kupika duniani uitwao Global eCooking Coalition (GeCCo) wakati wa Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi jijini Nairobi.
“Umeme kwa kawaida umechukuliiwa na Wakenya kuwa njia mbadala ya kupika ambayo ni ghali. Familia za kipato cha kati mara nyingi zinakuwa na vyombo mahususi vya kupikia kama birika na mikrowevu lakini zinategemea gesi ya petroli ya kimiminika kupikia. Lakini hali imebadilika kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni. Kwa hivyo, kuna uwezo mkubwa wa umeme kutumiwa kupikia nchini, uwezo ambao haujatumiwa ipasavyo,” alisema Mhandisi Siror.
Data za hivi karibuni zinaashiria kuwa ni asilimiia moja tu ya wateja wa kampuni ya Kenya Power wanaotumia umeme kupikia huku wengi wakitumia kuni na gesi.
GeCCo ni mpango unaolenga kuharakisha mpito kutoka mbinu za kawaida za kupikia na badala yake kutumia umeme kupikia kwa matumizi ya nyumbani na kibiashara.
“Kenya Power itafanya kazi na washirika wake kuhamasisha matumizi ya umeme katika kupika kote nchini,” amesema Mhandisi Siror.
Kupitia kampeni yake ya uhamasishaji wa umma ya Pika na Umeme, Kenya Power inalenga kuongeza matumizi ya umeme katika upishi miongoni mwa wateja wake.
Kampuni hiyo imeanzisha vituo vya kunadi matumizi hayo katika kaunti za Nairobi, Kisumu, Nakuru, na Mombasa ili kupigia debe matumizi ya umeme kupikia kote nchini.