Kenya na Uholanzi zimetia saini Mikaba mitatu ya Maelewano na Barua ya Dhamira ambayo itaboresha biashara kati ya nchi hizo mbili.
Mikataba hiyo ilitiwa saini katika Ikulu ya Nairobi wakati wa kuanza kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu nchini Kenya ya Mfalme Willem Alexander na Malkia Máxima wa Uholanzi.
Wakati wa mkutano wa pamoja na wanahabari, Rais William Ruto alisema: “Uongozi wa Uholanzi duniani katika kilimo endelevu, usimamizi wa maji na nishati mbadala unawiana na maono ya Kenya ya mwaka 2030.”
Mfalme Alexander alipongeza uhusiano thabiti na wa kirafiki uliopo kati ya Kenya na Uholanzi ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 60.
“Tunatoa umuhimu mkubwa kwa ushirikiano wetu na Kenya,” alisema Mfalme Alexander wakati wa mkutano huo na wanahabari.
“Ziara hii inaonyesha namna maslahi yetu yanavyowiana na namna uhusiano wetu umekuwa wa karibu.”
Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki, Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi, Mawaziri, Makatibu na viongiozi wengine.
Mikataba hiyo ya Maelewano ni juu ya Kamati ya Pamoja ya Biashara itakayokuza biashara kati ya nchi hizo mbili na Kundi Kazi la Masharti ya Utendakazi inayolenga kuboresha kilimo kati ya nchi hizo mbili.
Mkataba mwingine uliotiwa saini ni ule wa kukuza ushirikiano wa utalii kwa kuhamasisha watalii zaidi kutoka Uholanzi kuitembelea Kenya na wafanyabiashara wengi zaidi Waholanzi kuwekeza katika sekta ya utalii humu nchini.
Barua ya Dhamira ni kutoka kwa kampuni ya Uholanzi ya Invest International kufadhili miradi miwili ya maji, mradi mmoja mjini Naivasha na mwingine kule Sabaki.
Rais Ruto alisema: “Miradi hii itaongeza upatikanaji wa maji safi ambao ni mhimili muhimu kwa maendeleo endelevu na ukuaji uchumi.”