Mkuu wa mawaziri ambaye pia ni Waziri wa mambo ya nje Daktari Musalia Mudavadi ameashiria msimamo thabiti wa Kenya wa kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia kuboresha miamala na nchi zote wanachama.
Mudavadi amesema hayo alipokutana na waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Daktari January Makamba pembezoni mwa kikao cha 19 cha Jumuiya ya NAM ngazi za mawaziri katika eneo la Munyonyo nchini Uganda.
Mawaziri hao wawili wa mambo ya nje nchini Kenya na Tanzania wamekubaliana kuongoza juhudi za kupanua wigo wa ushirikiano kati ya mataifa haya mawili na kutatua migogoro yoyote kupitia njia za kidiplomasia siku za usoni.
Mkutano huu umefanyika siku moja tu baada yao kutatua mgogoro wa safari za ndege kati ya Nairobi na Dar es Salaam uliotishia kuathiri biashara ya pande mbili.
“Undugu wetu ni wa jadi na wenye uzito wa kipekee. Uhusiano wetu umekuwa ukitumiwa kama mfano bora na majirani wetu ndani na nje ya Afrika na hatuna sababu ya kuvuruga ukweli huu” alisema Mudavadi.
Waziri Makamba kwa upande wake alisema “Sisi ni kama pacha, mmoja akiugua, mwenzake hupata maumivu pia. Zipo changamoto hapa na pale na hilo ni jambo la kawaida. Utatuzi wa changamoto hizi unapaswa kuongozwa na busara na hekima ya upeo wa juu na mimi na wewe tumekomaa katika uga huo.”
Kenya na Tanzania pia zimekubaliana kushirikiana zaidi katika masuala ya usalama hasa kutokana na migogoro ya mashariki mwa Congo kwa upande wa Tanzania na tishio la ugaidi kutoka kwa makundi yenye misimamo mikali nchini Somalia kwa upande wa Kenya.
Marais wa nchi wanachama wa NAM watakuwa na kikao chao Ijumaa na Rais William Ruto anatarajiwa kuhudhuria.