Kenya itawatuza watu 264 waliochangia pakubwa kwa maendeleio ya taifa hili, kwenye sherehe za Siku Kuu ya Mashujaa itakayoandaliwa katika uwanja wa Kipchoge Keino kaunti ya Uasin Gishu.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Kitaifa la Mashujaa Charles Wambia, alisema baraza hilo limewatambua watu ambao walijitolea mhanga kuhudumia nchi hii, huku michango yao ikifanikisha taifa hili kupiga hatua za kimaendeleo.
Sherehe hizo zitakazoongozwa na Rais William Ruto, na kuandaliwa kwa ushirikiano wa kaunti tatu ambazo ni Uasin Gishu, Nandi na Elgeyo-Marakwet, zitaangazia nyanja tatu muhimu za usalama, michezo na uchumi.
Watakaotuzwa watatoka katika vitengo vya uongozi wa kidini, utamaduni, sanaa, michezo na ufadhili wa elimu, miongoni mwa vingine.
Ni mara ya kwanza kwa sherehe hizo kuandaliwa kwa ushirikiano wa kaunti tatu.