Akitoa hukumu hiyo siku ya Jumatatu katika Mahakama Kuu ya Mombasa, Lady Justice Diana Kavedza alisema kanisa la Makenzi la Good News International liliendesha shughuli zake kama kanisa lenye imani potovu, kutumia mafunzo ya kidini na mifumo ya uongozi ya kuwaagiza wafuasi kujinyima chakula hadi kufa wakijiandaa kwa mwisho wa dunia.
“Ushahidi ulio mbele yangu unabaini kuwa wafuasi wa Mackenzie kwanza walisajiliwa kupitia mfumo wa mawasiliano wa kidini. Waliagizwa kuhama. Walipowasili katika eneo hilo, walilazimishwa kususia chakula,” alisema Jaji Kavedza.

Aidha, mahakama hiyo ilifahamishwa kuwa watoto ndio waliokuwa wa kwanza kulengwa huku wengine wao wakinyimwa chakula, kuzuiwa na kuadhibiwa kwa kujaribu kula chakula au kutoroka.
Walinzi katika eneo hilo yadaiwa walithibiti mienendo ya wafuasi katika mpango huo wa makao ili kuwazuia wafuasi kuondoka.
Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka iliwasilisha mashahidi 123, huku ushahidi wa kimatibabu ukionyesha vifo 76 vilitokana na njaa, ilhali vyanzi vya vifo 112 vikikosa kubainika. Hata hivyo vifo vingine vilihusishwa na majeraha ya kichwa na kunyongwa.
Hukumu hizo zimeashiria tukio kubwa kwenye kesi ya mauaji ambapo zaidi ya miili 400 imepatikana kufikia sasa.
Mackenzie na viongozi wengine wa kanisa hilo pia wanakabiliwa na kesi zingine zikiwemo, ugaidi na utoaji wa mafunzo ya itikadi kali.