Kenya imepanga kutuma kundi lingine la maafisa 300 wa polisi nchini Haiti kwa lengo la kuunga mkono juhudi za kikosi cha kimataifa cha kudumisha usalama nchini humo.
Kinara wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi amesema hatua hiyo hususan itasaidia kuimarisha juhudi za kukabiliana na magenge ya uhalifu katika mji mkuu wa nchi hiyo Port-au-Prince na maeneo jirani.
“Maafisa waliosalia wamepangiwa kuondoka mapema mwaka 2025 na kutoa fursa ya kuundwa kwa kikosi kamili cha Umoja wa Mataifa, UN baadaye mwakani,” alisema Mudavadi wakati wa mazungumzo ya pande mbili na Waziri Mkuu wa Bahamas Philip Davis.
Wakati wa mkutano kati yao, Mudavadi alizungumzia hatua zilizopigwa na Kenya nchini Haiti.
“Kikosi hicho tarayi kimefanikiwa kuleta uthabiti kwenye miundombinu muhimu ikiwa ni pamoja na viwanja vya ndege, hospitali ya kitaifa na miundombinu muhimu kadhaa na barabara kuu katika mji wote wa Port-au-Prince.”
Mudavadi sasa anatoa wito kwa washikadau wote hasa wale ambao awali waliahidi kutoa msaada sambamba na UN kufanya hivyo kwa kusudi la kupiga jeki shughuli za kikosi hicho nchini Haiti.
Davis alielezea shukrani zake kutokana na msaada wa Kenya katika kudhibiti hali ya usalama nchini Haiti.
Aliahidi kwamba nchi yake ya Bahamas pia itatuma maafisa 150 kusaidia kikosi hcha kudumisha usalama katika taifa hilo la Caribbean.