Katibu katika Wizara ya Kilimo Dkt. Paul Ronoh amesema kuwa Kenya inatarajia kurekodi ongezeko la mavuno ya mahindi mwaka huu, kufuatia ufanisi katika mpango wa usambazaji wa mbolea ya bei nafuu na serikali.
Ronoh ameusifia mpango huo akisema uliwadia wakati unaofaa na utamaliza tatizo la ukosefu wa chakula nchini.
Serikali ilisambaza zaidi ya magunia milioni 25 ya mbolea ya gharama nafuu kwa wakulima milioni 15 katika kipindi cha miaka miwili tangu mpango wa mbolea nafuu uanzishwe.
Pia Ronoh amefichua kuwa serikalli imo mbioni kujenga ghala za kuhifadhi nafaka katika halmashauri ya NCPB tayari kununua mahindi kutoka kwa wakulima.
Serikali pia itajenga ghala 100 za muda za kukausha mahindi kote nchini ili kuzuia kuharibika kwa nafaka na kupunguza hasara kwa wakulima.
Katibu huyo pia amewahakikishia wakulima kuwa ameweka mikakati ya kuhakikisha inanunua mahindi ya wakulima na pia mbegu zilizopasishwa pekee zinauziwa wakulima kwa msimu wa upanzi wa mwaka ujao.