Vijana wa Kenya watakwaruzana na Tanzania katika nusu fainali ya kwanza ya mashindano ya mwaka huu kuwania kombe la CECAFA kwa chipukizi walio chini ya umri wa miaka 18.
Mchuano huo utasakatwa hii leo katika uwanja wa Mamboleo katika kaunti ya Kisumu kuanzia saa nane na nusu alasiri.
Kisha baadaye, vijana wa Uganda watachuana na Rwanda katika mchuano wa pili wa nusu fainali.
Kenya ilifuzu kwa nusu fainali baada ya kuongoza kundi A kwa alama 9 wakifuatwa na Rwanda kwa alama 6.
Waziri wa Michezo Ababu Namwamba ametoa wito kwa vijana hao kujituma na kuhakikisha wanawalaza mahasimu wao kutoka nchi jirani ya Tanzania.
Uganda waliongoza kundi B kwa alama 6 baada ya kuwalemea Sudan Kusini magoli 2 kwa nunge katika mechi ya mwisho iliyochezwa Jumamosi iliyopita.
Tanzania nao walifuzu kwa nusu fainali baada ya kutoka sare ya bao 1 dhidi ya Zanzibar katika mchuano wa mwisho.
Tanzania na Zanzibar walitoshana alama, magoli ya kufunga na ya kufungwa, na ikabidi nidhamu itumike kuwatenganisha ndugu hao ndiposa Tanzania wakawahi tiketi.
Mashindano hayo yalichukua mapumziko Jumapili na Jumatatu, na yatarejea hii leo huku mechi za nusu fainali zikisakatwa.
Fainali ya mashindano hayo itapigwa Ijumaa wiki hii.