Timu ya taifa ya Kenya ya Voliboli ya wanawake-Malkia Strikers,itashuka katika uwanja wa Kasarani kupambana na Misri katika fainali ya kuwania Kombe la Afrika leo Ijumaa,kuanzia saa kumi na mbili jioni.
Kenya ilijikatia tiketi kwa fainali kufuatia ushindi wa seti 3-0, dhidi ya Cameroon, katika nusu fainali Alhamisi usiku katika ukumbi wa Kasarani.
Malkia Strikers wakibebwa na mashabiki wa nyumbani waliibwaga Cameroopn seti 3-0, katika nusu fainali kwa alama za 25-19,25-20 na 25-20.
Misri pia waliingia fainali baada ya kuwaangusha Rwanda seti 3-0 za 25-5,25-17 na 32-30, katika nusu fainali ya kwanza.
Rwanda na Cameroon watakutana Ijumaa kuwania nafasi ya tatu na nne.
Mshindi wa fainali ya Jumamosi atafuzu kuiwakilisha Afrika katika mashindano ya Dunia mwaka ujao na Michezo ya Olimpiki mwaka 2028 nchini Marekani.
Rais wa shirikisho la Voliboli Ulimwenguni (FIVB) Fabio Azevedo,Rais wa shirikisho la Voliboli Afrika (CAVB) Hajij Bouchra,Waziri wa michezo Salima Mvurya na katibu wake Elijah Mwangi, walihudhuria nusu fainali ya Kenya dhidi ya Cameroon.
Aidha,Waziri Mvurya ametangaza kuituza timu hiyo shilingi milioni 1 kwa kufuzu kwa fainali huku akiahidi kuwa Rais Ruto ataituzwa endapo watatwaa ubingwa.