Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, amesema Kenya itaendela kuunga mkono afisi za Umoja wa Mataifa Jiji Nairobi pamoja na mfumo mzima wa UN.
Akizungumza afisini mwake Jijini Nairobi alipompokea Mshirikishi Mteule wa UN hapa nchini Garry Conille, Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje alisema Kenya inaendelea kupigia debe ushirikiano kupitia majukwaa, kama vile Jukwa kuhusu Maendeleo ambalo huwiainisha misaada katika sekta muhimu kama vile Kilimo, Nishati, Miundombinu, Nyumba na kukabiliana na Tabianchi.
Mudavadi alimpongeza Conille kwa kuteuliwa kwenye wadhifa huo, akisema kuwa analeta tajiriba ya kupigiwa mfano kwenye afisi hiyo.
“Huku akiwa na uzoefu katika uongozi, analeta uwezo mkubwa wa kuimarisha ushirikiano wa Kenya na UN,” alisema Mudavadi kwenye ukurasa wake wa X.
Aidha, Mudavadi alimpongeza mtangulizi wa Conille, akimshukuru kwa mchango wake hapa nchini, akimtakia heri njema katika majukumu yake ya baadaye.
“Pamoja tutaendelea kuimarisha ushirikiano unaoiwezesha Kenya kuwa uchumi wenye ushindani zaidi hapa nchini,” aliongeza Mudavadi.