Waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo Mutahi Kagwe, amesema Kenya huagiza mayai bilioni tano kila mwaka kuziba nakisi ya zao hilo hapa nchini.
Kulingana na waziri huyo, taifa hili huzalisha mayai bilioni nne kila mwaka, dhidi ya hitaji la mayai bilioni 9 lililopo, akionya kuwa uagizaji mayai unapaswa kukomeshwa na kuongeza uzalishaji wa zao hilo muhimu.
Akizungumza alipozuru kituo cha Utafiti wa maziwa kwenye Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo (KALRO) eneo la Msabaha, kaunti ya Kilifi, waziri huyo alisema Kenya itaafikia utoshelevu wa chakula kupitia utafiti, sera zinazoongozwa na deta na ukulima unaozingatia sayansi.
“Tunapswa kukoma kuagiza mayai kutoka nje na kuanza kuimarisha uzalishaji wa zao hilo wenyewe. Hilo linahitaji kutekeleza kilimo kinachoongozwa na sayansi na wala sio kubahatisha,” alisema waziri Kagwe.
Aidha waziri huyo alidokeza kuwa kwa kuzingatia idadi ya watu inayoongezeka, wakulima wanapaswa kutumia mbinu za kisasa za kilimo kuhakikisha ongezeko la mazao.
Kagwe alitoa wito kwa vijana kukumbatia kilimo, akisema umri wastani wa mkulima wa Kenya ni miaka 64.
