Kenya imejitolea kukuza uhusiano wake na China, asema Mudavadi

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi (Kushoto), na balozi wa China hapa nchini Zhou Pingjian (Kulia).

Serikali itachukua hatua za kuimarisha uwekezaji wa kibinafsi wa China katika sekta zingine za nchi hii mbali na miradi ya barabara.

Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi alidokeza kuwa China ni mshirika mkuu wa Kenya wa kimaendeleo, akisema taifa hilo linalenga kuwekeza kwa miradi hapa nchini.

“Hatua hii ya kimaksudi inalenga kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Kenya na China, na kuhakikisha ushirikiano huo unawaleta raia wa mataifa hayo pamoja,” alisema Mudavadi.

Kulingana na waziri huyo wa mambo ya nje, sekta kama vile ya habari na mawasiliano ICT,  kawi safi, elimu, utafiti wa pamoja, hoteli na nyumba, zimenufaika pakubwa kutoka kwa serikali ya Uchina na kuhusishwa kwa sekta ya kibinafsi ya China.

Mudavadi aliyasema haya wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 75 ya Jamuhuri ya taifa ya watu wa China, zilizoandaliwa jijini Nairobi.

Alikariri jukumu muhimu ambalo uwekezaji wa China umetekeleza katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Kenya.

Waziri huyo alisifu urafiki wa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili akisema umesaidia kuleta maendeleo humu nchini.

Kwa upande wake balozi wa China hapa nchini Zhou Pingjian, aliangazia utamaduni wa urafiki uliopo kati ya nchi hizi mbili, huku akihimiza haja ya ushirikiano zaidi kwa manufaa ya watu wa nchi hizi mbili.

Share This Article