Kega atishia kwenda mahakamani Jubilee isipohusishwa kwenye majadiliano

Marion Bosire
2 Min Read

Mbunge wa bunge la Afrika Mashariki Kanini Kega ametishia kuelekea mahakamani iwapo chama cha Jubilee hakitahusishwa kwenye mazungumzo ya pande mbili kati ya muungano wa Kenya Kwanza na ule wa Azimio la Umoja One Kenya.

Kupitia taarifa, Kega alisema chama cha Jubilee ndicho nambari tatu kwa ukubwa kati ya vyama vya kisiasa nchini Kenya na hivyo lazima kihusishwe.

Taarifa ya Kega inajiri wakati ambapo kuna mjadala bungeni wa kuratibu kamati ya kitaifa ya mazungumzo ya pande mbili ili kuyahalalisha.

Mjadala huo uliofikishwa bungeni na kiongozi wa walio wengi Kimani Ichung’wa na mwenzake wa upande wa walio wachache Opiyo Wandayi umeorodhesha masharti ya mazungumzo hayo ambayo yataendelea kwa siku 60 zijazo.

Masharti hayo yanajumuisha wakati ambapo kamati hiyo inatarajiwa kutoa ripoti ya mwisho kwa viongozi wa mirengo hiyo miwili ya kisiasa na kufikishwa bungeni pia ili kupitishwa.

Kamati hiyo imekubali kupokea maoni ya umma, mashirika ya kitaalamu na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yatazingatiwa.

Mjadala wa kuhalalisha kamati ya mazungumzo ya pande mbili utaandaliwa katika bunge la kitaifa leo alasiri.

Wawakilishi wa muungano wa Azimio kwenye kamati hiyo ni kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa walio wachache bungeni Opiyo Wandayi, kiongozi wa chama cha DAP Eugene Wamalwa, seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni na mbunge wa Malindi Amina Mnyazi.

Kenya Kwanza inawakilishwa na kiongozi wa wengi bungeni Kimani Inchung’wa, kiongozi wa wengi katika bunge la seneti Aaron Cheruiyot, gavana wa kaunti ya Embu Cecily Mbarire, mbunge wa bunge la Afrika Mashariki Hassan Omar na mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Bungoma Catherine Wambilianga.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *