KCB wamesajili ushindi wa seti 3 kwa moja dhidi ya timu ya DCI, katika mechi ya mkondo wa nne wa ligi kuu ya shirikisho la Voliboli siku ya Jumamosi katika uwanja wa taifa wa Nyayo.
Mabingwa wa zamani wa Afrika KCB, walisajili ushindi wa alama 25-21 katika seti ya kwanza, kabla ya kupoteza seti ya pili kwa alama sawa 21-25.
Hata hivyo KCB waligutuka na kuwaparuza DCI pointi 25-19 na 25-18 katika seti zilizofuatia mbili.
“Tulianza vyema katika seti ya kwanza lakini seti ya pili haikuwa nzuri kwani tulifanya makosa mengi na kuchangia kupoteza.
Hata hivyo tulijikakamua na kutwaa ushindi katika seti mbili za mwisho .
Ushindi wa leo ni muhimu kwetu kwani unainua morali huku tukijiandaa kwa mechi ngumu kesho” akasema mahodha wa KCB Edith Wisa.
KCB watashuka uwanjani Jumapili kwa mechi ngumu dhidi ya Kenya Pipeline.