Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, NCIC, imezindua mkakati mpya unaolenga kuzuia maandamano sawia na yale yaliyoshuhudiwa hapa nchini mwaka uliopita.
Nguzo kuu katika mpango huo, ni kutiwa saini kwa mkataba wa maelewano kati ya NCIC na Shirika la Utangazaji nchini ,KBC, upigia debe mazungumzo baina ya vizazi vya hapa nchini.
Kama sehemu ya makubaliano hayo, mashirika hayo mawili, yataandaa mikutano ya mazungumzo katika muda wa miaka miwili ijayo katika kaunti zote 47, kwa lengo la kudumisha amani na kuimarisha umoja wa kitaifa.
Wakati wa kutiwa saini kwa makubaliano hayo katika afisi za KBC, Mkurugenzi Mkuu wa KBC Agnes Kalekye alitoa wito kwa Wakenya kushiriki kikamilifu mikutano hiyo ya mazungumzo, akithibitisha kuwa mikutano hiyo itapeperushwa kupitia runinga, redio na majukwaa yote ya dijitali yanayomilikiwa na KBC.
Alikariri jukumu kuu linalotekelezwa na vyombo vya habari katika kudumsha amani hapa nchini.
Kwa upande wake, kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa NCIC Harrison Kariuki, alithibitisha kuwa tume hiyo imejitolea kuimarisha mazungumzo hayo baina ya vizazi ili kuziba mianya hapa nchini hasaa baada ya kuzuka kwa maandamano yaliyoandaliwa na vijana wa Gen Z mwaka jana.