KBC inahitaji kufanyiwa mabadiliko makubwa, asema Kabogo

Martin Mwanje
1 Min Read
William Kabogo - Waziri mteule wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali wakati akisailiwa na kamati ya bunge

Shirika la Utangazaji nchini, KBC linahitaji kufanyiwa mabadiliko makubwa ili kuboresha utenda kazi wake kwa lengo la kukidhi mahitaji ya umma. 

Mabadiliko hayo yanapaswa kufanywa kwa kupigia darubini namna ambavyo shirika hilo limekuwa likiendesha shughuli zake siku zilizopita.

Akizungumza wakati akisailiwa na Kamati ya Uteuzi ya Bunge la Taifa leo Jumanne alasiri, Kabogo amependekeza kuwa ili kupiga dafrau changamoto za kifedha zinazolikabili shirika hilo kwa sasa, kuna haja ya kuanzisha vitengo viwili vya utenda kazi.

Alisema kitengo kimoja kinapaswa kujishughulisha na masuala ya utangazaji wa umma wakati kingine kikijishughulisha na masuala ya biashara.

Aidha, Kabogo amesema kuna haja ya kutathmini vifaa ilivyo navyo KBC na kubaini vile inavyohitaji.

Kulingana naye, ikiwezekana vifaa vipya vinaweza kukodiwa katika hatua anayosema itapungua gharama ya ununuzi ikizingatiwa matumizi ya vifaa hivyo huisha baada ya takriban miaka mitano.

Kadhalika ameahidi kuhakikisha kuwa huduma zote za serikali zinapatikana mtandaoni ili kuboresha utenda kazi wa serikali.

Kabogo ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali kuchukua wadhifa ambao awali ulishikiliwa na Dkt. Margaret Ndung’u.

Dkt. Ndung’u alikuwa ameteuliwa kuwa Balozi wa Kenya nchini Ghana ingawa alikataa uteuzi huo akitaja sababu za kibinafsi.

 

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *