Hatua ya serikali ya kukodisha uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta JKIA kwa wawekezaji wa kibinafsi, imepingwa vikali na chama cha wafanyakazi wa viwanja vya ndege humu nchini KAWU.
Kikipinga hatua hiyo, chama hicho kilisema halmashauri ya kusimamia viwanja vya ndege humu nchini KAA, haikutekeleza ipasavyo vikao vya kushirikisha umma kuhusu pendekezo la kutoa kibali kwa kampuni ya kibinafsi kuhusu usimamizi wa uwanja huo wa ndege na kimetishia kugoma iwapo mpango huo utafaulu.
“Hatujawai husishwa kama chama na wawakilishi wa wafanyakazi,” alisema Ndiema.
Haya yanajiri huku haari zikifichuliwa kuwa kuna mpango wa kukodisha uwanja wa JKIA kwa kampuni ya kibinafsi ya Adani, ili kusimamia shughuli za uwanja huo kwa muda wa miongo mitatu.
Katibu mkuu wa chama cha KAWU Moss Ndiema, alisema halmashauri ya kusimamia viwanja vya ndege hapa nchini KAA, ina rasilimali na uwezo wa kutosha wa kusimamia ipasavyo shughuli za uwanja wa JKIA.
Ndiema aliongeza kuwa mipango yoyote ya kuleta mwekezaji wa kibinafsi, inapaswa kuangaziwa kwa ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa kimataifa.
Kampuni ya Adani inadaiwa kuwa inalenga kuwekeza dola bilioni 1.9 katika uwekezaji huo.
Ndiema alisema mpango huo unatishia maisha ya wafanyakazi wengi na wategemezi wao.
Hata hivyo, serikali imewahakikishia wakenya kwamba uwanja wa JKIA ni rasilimali ya kimkakati ya kitaifa ambayo haitauzwa.
Hivi majuzi maandamano yaliandaliwa hapa nchini kupinga mipango yoyote ya kuuza uwanja huo wa ndege, baada ya uvumi kuibuka kuwa, kulikuwa na mipango ya kuuza uwanja huo.