Katibu Omollo awataka Machifu kuongoza upanzi wa miche kote nchini

Martin Mwanje
2 Min Read

Serikali imezindua mpango wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi unaolenga kupanda miche zaidi ya milioni moja kila mwezi kote nchini.  

Mpango huo utaongozwa na Machifu wote 3,950 katika ngazi ya kata.

Unakuja wakati ambapo Rais William Ruto ameagiza kupandwa kwa miche bilioni 15 kufikia mwaka 2032.

Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo ameongoza uzinduzi wa mpango huo kwenye shule ya msingi ya Nderi, kaunti ndogo ya Kikuyu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Omollo alilalamikia athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na ukame wa muda mrefu na mafuriko ya mara kwa mara katika baadhi ya maeneo ya nchi.

Kulingana naye, mabadiliko ya tabia nchi ni tishio kwa usalama wa taifa na juhudi za kuleta amani nchini. na kusisitiza umuhimu wa umoja katika kuikabili hali hiyo.

“Bila shaka, tunatambua kuwa amani, usalama na mabadiliko ya tabia nchi vina uhusiano wa karibu. Nchini Kenya, tunakumbana na hatari nyingi kwa amani na usalama zinazohusiana na tabia nchi.”

Alitoa mfano wa ukame wa muda mrefu ambao alisema umesababisha migogoro miongoni mwa jamii zinazoshindania rasilimali adimu kama vile maji, malisho na chakula.

Chini ya mpango mpya uliozinduliwa, Wizara ya Usalama wa Kitaifa itamsaidia kila Chifu kuzileta pamoja jamii zao na kuratibu upanzi wa miche isiyopungua 250 Ijumaa ya kwanza ya kila mwezi.

Dkt. Omollo alisema Machifu wote watafuatilia na kuripoti hatua iliyopigwa ili kuhakikisha miche hiyo inatunzwa vizuri.

Ametoa wito kwa Wakenya kuunga mkono juhudi za Machifu hao kufanikisha mpango huo.

 

Website |  + posts
Share This Article