Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, UN Antonio Guterres ameelezea kusikitishwa kwake kutokana na ripoti za mauaji na kujeruhiwa kwa watu kadhaa wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024 jana Jumanne.
Ametaka maandamano yote nchini humo kufanyika kwa njia ya amani.
Ripoti ambazo hazijathibitishwa rasmi na mamlaka za Kenya zinasema takriban watu 8 walifariki na mamia ya wengine kujeruhiwa wakati wa maandamano ya jana Jumanne.
“Nimehuzunishwa mno na ripoti za vifo na majeruhi – wakiwemo wanahabari na matabibu – zinazohusiana na maandamano nchini Kenya,” alisema Guterres katika mtandao wake wa X.
“Natoa wito kwa mamlaka za Kenya kujizuia, na kutoa wito kwa maandamano yote kufanyika kwa njia ya amani.”
Matamshi yake yanakuja wakati ambapo kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ametoa wito kwa Jumuiya ya Afrika, EAC, Umoja wa Afrika, AU na UN kuingilia kati ili kuepusha athari za machafuko yanayoshuhudiwa nchini humo.