Viongozi Martha Karua wa chama cha Narc K na Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper wametofautiana kuhusiana na uundwaji wa Kamwene.
Kamwene ni vuguvugu la kisiasa linalowaleta pamoja viongozi wa kisiasa kutoka eneo la Mlima Kenya akiwemo Karua.
Kulingana na Kalonzo, Kamwene ni “sera binafsi ya kutisha ya kikabila na kisiasa isiyoweza kwenda popote.
“Ningewashauri marafiki zangu kuachana nayo na tudumishe umoja wetu,” alisema Kalonzo wakati akihojiwa na runinga moja nchini.
Karua anashangaa ni kwa nini vuguvugu la Kamwene linamkosesha Kalonzo usingizi.
“Mbona Kamwene inamtia hofu Kalonzo Musyoka kiasi kwamba anaizungumzia mara kwa mara?” alihoji Karua katika mtandao wake wa X.
Kalonzo na Karua ni wanachama wa muungano wa Azimio.
Wawili hao wamechukua misimamo tofauti juu ya ripoti ya uwiano wa kitaifa iliyotayarishwa na kamati ambayo Kalonzo alikuwa mwenyekiti mwenza.
Huku Kalonzo akiunga mkono, Karua ameipuuzilia mbali ripoti hiyo akisema ilishindwa kuangazia suala muhimu la kupunguzwa kwa gharama ya juu ya maisha inayohangaisha Wakenya.
Msimamo sawia umechukuliwa na kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa.
Na huku Kalonzo akitangaza kuwa atagombea urais mwaka 2027 na Raila Odinga akionyesha dalili za kujaribu bahati tena kwa mara ya sita, huenda migawanyiko inaukodolea macho muungano wa Azimio.