Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz leo Jumatatu amefanya ziara ya kushtukiza katika nchi inayokumbwa na vita ya Ukraine na kusistiza tena msaada wa nchi yake kwa Ukraine katika mapambano yake dhidi ya Urusi.
Scholz ameahidi msaada zaidi wa dola milioni 680 utakaotolewa kabla ya mwisho wa mwaka huu na nchi yake ambayo ndio msambazaji mkubwa wa silaha kwa Ukraine barani Ulaya.
“Nimesafiri kuelekea nchini Ukraine usiku: kwa treni kupitia nchi ambayo imekuwa ikijilinda dhidi ya vita vya kichokozi vya Urusi kwa zaidi ya siku 1,000,” alisema Scholz kupitia mtandao wake wa X.
Aliongeza kwenye taarifa kuwa “Ukraine imekuwa ikijilinda kishujaa dhidi ya vita vya kichokozi visivyokuwa na huruma vya Urusi”.
“Kutokana na ziara yangu hapa jijini Kyiv, ningependa kuelezea kusimama kwangu na Ukraine,” aliongeza Scholz, atakayekabiliwa na uchaguzi mpya mwezi Februari mwakani.
“Ningependa kuweka bayana hapa kuwa Ujerumani itasalia muungaji mkono thabiti wa Ukraine barani Ulaya”.
“Katika mkutano wangu na Rais Volodymyr Zelensky, nitatangaza vifaa vingine zaidi vya kijeshi vyenye thamani ya yuro milioni 650, vitakavyotolewa mwezi Disemba. Ukraine sasa inaweza ikaitegemea Ujerumani — tunasema tunachokifanya. Na tunafanya tunachokisema.”