Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja ameachiliwa huru na Mahakama Kuu huku ikimpa onyo kali baada ya kumpata na hatia ya kudharau mahakama.
Haya yanatokana na hatua ya kufungwa kwa barabara na polisi jijini Nairobi wakati wa maandamano ya Juni 25, 2026.
Jaji Patricia Nyaundi alisema hakukuwa na nia wala manufaa ya kumpa Kanja adhabu kwa tukio la sasa, lakini akaonya kwamba mahakama haitasita kutoa adhabu kali zaidi ikiwa mwenendo huo utajirudia.
Jaji huyo alibainisha kuwa Kanja alifika mwenyewe mbele ya mahakama akiwa ameandamana na maafisa wakuu wa polisi, jambo ambalo alizingatia katika kuamua adhabu faafu.
Pia alizingatia ahadi yake ya kuhakikisha amri ya mahakama inawafikia maafisa walio chini ya uongozi wake, pamoja na uhakikisho wake kwamba ukiukaji huo hautajirudia.
Kanja alikuwa amepatikana binafsi na hatia ya kudharau mahakama baada ya polisi kuweka vizuizi na mabano ya barabarani katika maeneo mbalimbali ya Nairobi Juni 25 bila kutoa taarifa kwa umma ilivyohitajika chini ya amri ya awali ya mahakama.
Kesi ya kudharau mahakama ilitokana na amri ya muda ya mahakama iliyotolewa Julai 2025, iliyoitaka Huduma ya Kitaifa ya Polisi kuwafahamisha wananchi kabla ya kuweka vizuizi vya dharura au mabano ya barabarani.
Taasisi ya Katiba iliwasilisha kesi mahakamani baada ya polisi kuzuia ufikiaji wa jiji la Nairobi na barabara zingine kuu katika maadhimisho ya miaka miwili tangu maandamano ya Juni 25, 2024.