Kampuni inayoendesha programu ya teksi mitandaoni ya Bolt imesitisha mikataba na madereva wapatao elfu 5 nchini Kenya kufuatia kukosa kufuata kanuni za kazi na usalama.
Bolt ilielekezwa kuchukua hatua hiyo na mamlaka ya uchukuzi na usalama barabarani NTSA.
Hatua hiyo imekuwa ikitekelezwa katika muda wa miezi 6 iliyopita katika kile kinachoonekana kama hatua ya kutekeleza kanuni kali za usalama za NTSA.
Kampuni hiyo ambayo asili yake ni Estonia na inahudumu katika miji 15 nchini itawekeza shilingi milioni 20 katika mipango ya kiusalama.
NTSA ilikuwa imeomba Bolt ielezee jinsi itahakikisha usalama wa madereva na abiria hasa baada ya malalamishi kuibuliwa kila mara.
Kampuni hiyo sasa inasema kwamba imeandaa mpango wa kuhakikisha usalama wa madereva na wateja na kusimamisha tozo ambalo ilikuwa imeweka la kuitisha gari.
Tozo hilo lilikuwa limesababisha mafarakano kati ya madereva na wateja.
Chini ya mpango huo madereva watapata mafunzo na wahimizwe kuhakikisha utekelezaji wa kanuni za usalama na watakaokosa kuzitimiza wataondolewa.