Kambi ya walinzi wa baharini kuanzishwa katika kisiwa cha Mfangano

Tom Mathinji
1 Min Read
Katibu katika wizara ya usalama wa taifa Dkt. Raymond Omollo.

Serikali ina mipango ya kuanzisha kambi ya walinzi wa baharini katika kisiwa cha Mfangano kaunti ya Homa Bay, ili kukabiliana na maswala ya usalama katika ziwa Victoria.

Katibu katika wizara ya usalama wa kitaifa Dkt. Raymond Omollo, alisema hatua hiyo itatekelezwa hivi karibuni.

Kulingana na Omollo, uzinduzi wa kambi ya walinzi wa baharini katika kisiwa hicho, ni mojawepo wa ajenda za Rais William Ruto, kwa lengo la kuchochea uchumi wa baharini katika eneo la Nyanza.

“Wakati Rais alizuru eneo hili, wakazi walitaka kuanzishwe kwa kambi ya walinzi wa baharini, jukumu hilo liko katika wizara ya usalama na ninalishughulikia,” alisema Omollo.

Wavuvi katika ziwa Victoria wameripoti kushambuliwa katika ziwa hilo, wakati mwingi wakipoteza samaki walizotega pamoja na vifaa vyao.

Akizungumza siku ya Ijumaa wakati wa hafla ya kuchanga pesa katika shule ya upili ya Kakimba iliyoko katika kisiwa Mfangano Island, katibu huyo aliwahimiza wakazi wa Homa Bay kushirikiana na asasi za usalama ili kusaidia kuafikiwa kwa ajenda za Rais William Ruto, zilizotolewa wakati wa kampein za uchaguzi mkuu uliopita.

Huku akiwapongeza maafisa wa usalama katika eneo hilo, Omollo alisema serikali itaongeza maafisa zaidi wa usalama katika ziwa hilo, ambalo hutumika kuendesha biashara haramu.

Website |  + posts
Share This Article