Kamati ya bunge kuhusu usalama imekamilisha ziara ya kujifahamisha yanayoendelea katika kaunti ya Turkana na imeahidi kuangazia malalamishi ya wakazi.
Kulingana na naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Dido Rasso, kamati hiyo itatafuta suluhisho la kudumu kwa tatizo la ukosefu wa usalama katika eneo hilo.
Akizungumza katika maeneo mbalimbali ambapo wanachama wa kamati hiyo walifanya mikutano na wananchi, Rasso aliahidi kwamba masuala ya mizozo ya mipaka na kutumwa kwa polisi zaidi wa akiba katika kaunti ya Turkana yatapatiwa kipaumbele na kamati hiyo.
“Kama kamati, tuna wasiwasi kuhusu hali ya usalama katika kaunti ya Turkana. Tunachotafuta ni suluhisho la kudumu kwa sababu ni lazima tuishi na jamii nyingine kwani kila mmoja ana haki ya kuishi katika kaunti aliyozaliwa,” alisema Rasso.
Alipendekeza kutumwa kwa polisi zaidi wa akiba katika kaunti hiyo kutokana na ukubwa na utofauti wake.
Wabunge hao wanaonelea kwamba mizozo ya mipaka kati ya kaunti za Baringo na Pokot Magharibi na kati ya Kenya na Sudan Kusini na mzozo wa mpaka kati ya Kenya na Uganda, ndiyo imesababisha ukosefu wa usalama katika eneo hilo.
Mbunge wa Loima Protus Akuja, Mburu Kahangara wa Lari na Caroline Ngelechei walishangaa ni kwa nini wanajeshi wa KDF hawajawekwa katika viingilio vyote vya Kenya kama ilivyofanya Sudan kwa upande wao wa mpaka.
Walizitaka serikali za kaunti za maeneo yanayokumbwa na ukosefu wa usalama kununua magari yatakayotumiwa na maafisa wa usalama kama mchango wao kwa juhudi za kuimarisha usalama.
Walipata fursa ya kuhutubia polisi wa akiba waliosajiliwa hivi maajuzi ambao wanaendelea na mafunzo.