Kamati ya bunge kuhusu mawasiliano na ubunifu chini ya uenyekiti wa mbunge wa Dagoretti Kusini John Kiarie, ilimsaili mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya mawasiliano nchini CA avid Mugonyi kuhusu mpango mpya unaolenga kuimarisha maadili na ufuatiliaji wa ushuru wa rununu nchini Kenya.
Kamati hiyo ilitaka ufafanuzi kuhusu mpango huo na athari zake kwa ufaragha, utunzaji wa deta na namna ya kuutekeleza, hasa ikizingatiwa hofu ya deta ya watu binafsi kuangukia mikono isiyofaa.
Kiarie alikuwa na wasiwasi kuhusu sheria zilizopo za ufaragha na ufaafu wake katika kutunza deta ya wananchi wa Kenya.
“Tatizo sio usajili wa nambari za utambuzi wa rununu kimataifa (IMEIs). Ni nini haswa tunakubalia KRA kufikia kwenye simu ya mkenya chini ya kisingizio cha utunzaji deta?” aliuliza Kiarie.
Mbunge huyo aliangazia hatari kwamba wakenya watasusia miamala kwenye simu kwa kuogopa kufuatiliwa sana.
Geoffrey Wandeto mwanachama wa kamati hiyo aliibua maswali kuhusu uwezo wa CA wa kufuatilia na kutekeleza ufuatiliaji kwenye simu zote za rununu zinazoingia nchini ili kuhakikisha suala kama la Worldcoin halijirudii.
Mugonyi alielezea kwamba CA ilipokea agizo la Rais la kutekeleza mpango huo unaoangazia pakubwa maadili ya rununu na ufuatiliaji wa ushuru na wala sio ufuatiliaji wa miamala.
Mpango huo ulivyoundwa kulingana na Mugonyi utatuma jumbe kuhusu watumizi wa rununu wanaoanza kutumia rununu mpya bila kulipa ushuru.
Iwapo nambari ya utambuzi ya rununu hiyo haijasajiliwa, basi inazimwa na hivyo haiwezi kuunganishwa na mtandao wowote nchini, hadi ilipiwe ushuru.
Wandeto alitaka kujua pia jinsi mpango huo utaathiri wageni kutoka nchi nyingine akisema usafiri wao haufai kutatizwa.
Mugonyi alihakikishia kamati hiyo ya mawasiliano kwamba watalii na wanadiplomasia watapatiwa muda wa kutosha ambapo rununu zao zitaorodheshwa kama zisizohitajika kulipiwa ushuru.
Katibu wa utangazaji Edward Kisiangani, alitambua uwezekano wa mwingiliano wa ushuru kimataifa huku akipendekeza makubaliano ya ushiriki wa deta na nchi ambazo zitapendelea hilo.
Mamlaka ya mawasiliano – CA ilitoa ilani kwa umma Oktoba 24, 2024, iliyoelezea kuhusu utekelezaji wa mpango huo kuanzia Oktoba 31, 2024.