Kamala Harris akubali kushindwa huku Obama akipongeza Trump kwa ushindi

Marion Bosire
2 Min Read

Naibu Rais wa Amerika Kamala Harris amekubali kwamba ameshindwa na Donald Trump kwenye uchaguzi wa mwaka huu wa 2024.

Alisema hayo alipohutubia wafuasi wake waliokuwa wamekusanyika katika chuo kikuu cha Howard Jumatano.

Wakati huo huo, Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama wa chama cha democratic na mmoja wa waliokuwa wakimuunga mkono kwa dhati Kamala, amempongeza Donald Trump na JD Vance kwa kuibula washindi wa kinyang’anyiro cha urais.

Kupitia taarifa kiongozi huyo alisema kwamba hawakutarajia matokeo hayo kwa sababu hawakubaliani na sera za chama cha Republican.

“Lakini kuishi katika demokrasia, ni kutambua kwamba maoni yetu hayatashinda kila wakati. Lazima tuwe tayari kubadilishana mamlaka kwa njia ya amani.” alisema Obama.

Aliendelea kusema kwamba yeye na mke wake Michelle wanajivunia Kamala Harris na mgombea mwenza Tim Walz wa chama chao cha Democratic kwa kuendesha kampeni nzuri.

Shukrani zake ni kwa wahusika wote waliojitolea kuhudumu kwenye kampeni ya wawaniaji hao.

Kulingana na Obama, matatizo yanayokumba taifa la Amerika yanaweza kusuluhishwa, lakini hilo linaweza kuafikiwa tu kupitia kusikilizana na kwa kufuata kanuni za katiba na za demokrasia ambazo anasema zimeifanya nchi hiyo kuwa bora.

Taarifa ya Obama wa chama cha Democrat inajiri baada ya Trump kutangazwa rasmi kuwa mshindi katika uchaguzi mkuu wa Amerika ambapo alijizolea kura zaidi ya 290 za majimbo ikilinganishwa na za Harris ambazo ni 223.

Hii ni mara ya pili Trump anashinda mwaniaji wa kike wa chama cha democratic, baada ya kumshinda Hillary Clinton kwenye uchaguzi wa mwaka 2016.

Share This Article