Hali ya huzuni ilighubika kijiji cha Emureko, eneo bunge la Butere kaunti ya Kakamega, baada ya kaka wawili kuuawa na majambazi.
Majambazi hao waliokuwa wamejihami kwa silaha butu, walivamia makazi ya kaka hao kabla ya kuwaua.
Kulingana na ripoti ya polisi, mmoja wa wahasiriwa hao alikuwa mzee wa kijiji aliyehusika na juhudi za kukabiliana na uhalifu, swala linaloshukiwa kuwa lilisababisha majangili hao kutekeleza uovu huo.
Jane Auma, mjane wa Thomas Eshapaya, mwenye umri wa miaka 46, alisema majangili hao walivamia nyumba yao saa nne usiku, huku juhudi zao za kuitisha usaidizi zikikosa kuzaa matunda.
Linet Nangoye, mke wa kakake Eshapaya, alisema mume wake alienda kumsaidia ndugu yake aliposikia kamsa, lakini majangili hao wakamvamia.
Wakazi wa eneo hilo wamelalamikia ongezeko la visa vya wizi, huku wakiwashutumu polisi kwa utepetevu.
Mkuu wa polisi eneo bunge la Butere Julius Kiptoo, alithibitisha tukio hilo, na kuwahakikishia wakazi kwamba uchunguzi unaendelea ili kuwakamata wahuni hao.