Kabogo, Kagwe na Kinyanjui waapishwa kuwa Mawaziri

Katika sherehe hiyo, Rais Ruto alielezea imani aliyo nayo katika mawaziri hao kupitia ujuzi na tajiriba walizo nazo.

Tom Mathinji
2 Min Read
Kabogo,Kinyanjui na Kagwe waapishwa kuwa mawaziri.

Rais William Ruto leo Ijumaa aliongoza sherehe ya kuwaapisha mawaziri watatu wapya katika Ikulu ya Nairobi.

Mutahi Kagwe aliapishwa kuwa Waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo, Lee Kinyanjui akaapishwa kuwa Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda huku William Kabogo akiapishwa kuwa waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali.

Watatu hao waliapishwa baada ya uteuzi wao kuidhinishwa na bunge la taifa kufuatia zoezi la usaili lililolenga kubainisha ufaafu wao katika nyadhifa hizo.

Katika sherehe hiyo, Rais Ruto alielezea imani aliyo nayo katika mawaziri hao kupitia ujuzi na tajiriba walizo nazo.

“Mawaziri hawa watatu wana tajiriba katika utumishi wa umma. Kwa sababu hiyo, nina imani katika ujuzi na uwezo wao kwenye majukumu yao mapya,” alisema Rais Ruto.

Kiongozi wa taifa aliongeza kuwa watatu hao watachangia pakubwa katika mikakati inayoendelea ya kuimarisha uchumi wa taifa hili kutoka chini, inayolenga kukabiliana na changamoto za kiuchumi.

“Ninatarajia kuwa mtawahudumia Wakenya kwa kujitolea, utaalam, kwa usawa na uelewa. Tunapaswa kujizatiti kupunguza kutoelewana na kuwajumuisha Wakenya wote katika mageuzi ya kitaifa,” aliongeza Ruto.

Kagwe aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Afya katika serikali ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta huku Kinyanjui na Kabogo wakiwa Magavana wa zamani.

Watatu hao waliteuliwa na Rais Ruto mwezi Disemba mwaka 2024, alipotangaza mabadiliko katika utawala wake.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *