Junior Pope akumbukwa mwaka mmoja tangu alipoaga dunia

Pope na watu wengine wanne walifariki Aprili 10, 2024, baada ya mashua waliyokuwa wakisafiria kuzama kwenye mto Niger katika jimbo la Anambra

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji wa filamu za Nigeria almaarufu Nollywood Junior Pope amekumbukwa na wengi mitandaoni mwaka mmoja tangu alipoaga dunia.

Mke wake kwa jina Jennifer Odonwodo alichapisha picha akiwa na watoto wao watatu na nyuma yao ni picha kubwa ya mwendazake, huku akielezea jinsi maisha yamekuwa magumu bila yeye.

“Umekuwa mwaka mmoja wa kuvumilia hasara isiyoelezeka na hakuna siku hata moja imepita bila kukuwaza wewe.” aliandika mama huyo wa watoto watatu wa kiume.

Jennifer ambaye ni mfanyabiashara alielezea jinsi wanawe wamekuwa wakimuuliza maswali mengi hasa kuhusu mambo mbali mbali ambayo walikuwa wameahidiwa na baba yao kabla ya kifo chake cha ghafla.

“Bado sijapata maneno sahihi ya kujibu Jason na Jaden wanaotaka kujua iwapo baba atatimiza ahadi ya kuwapeleka katika taasisi nzuri ya soka na awepo wakati wa mechi yao ya kwanza rasmi.” alisema Jennifer.

Kitindamimba naye kwa jina Jamon au J Papa anataka kujua ni lini baba atamletea kijigari cha kuchezea.

Waigizaji wengine wa Nollywood pia wamemkumbuka Junior Pope leo huku wengi wakichapisha picha zake za awali na wengine wakichapisha picha aliyotoa mke wake.

Calista Okoronkwo aliandika, “Mwaka mmoja uliopita, uliondoka hapa ulimwenguni. Ninahisi kana kwamba ni jana, endelea kupumzika kifuani mwa Mungu.”

Mwigizaji huyo aliwataja pia watu wanne waliofariki pamoja na Junior Pope, Aprili 10, 2024, siku ambayo anasema hatawahi kuisahau.

Ekene Umenwa naye alimkumbuka akisema kwamba deni lake ambalo wamesalia nalo ni kutunza familia yake. “Deni lako tulilonalo ni kuitunza familia yako kwa sababu uliipenda sana na hilo ndilo ninataka kila mmoja afahamu.” aliandika.

Umenwa aliendelea kwa kumtia moyo Jennifer akimwambia kwamba Mungu yuko naye siku zote na anaomba ampe nguvu na busara ya kuendeleza jukumu lake kama mzazi.

Junior Pope ambaye jina lake halisi ni John Paul Obumneme Odonwodo wa wahudumu wengine wanne wa shughuli za uandaaji wa filamu, walikufa maji Aprili 10, 2024, baada ya mashua waliyokuwa wakisafiria kuzama kwenye mto Niger katika jimbo la Anamra.

Website |  + posts
Share This Article