Juma Jux kufunga ndoa na Priscilla Ojo mwakani

Marion Bosire
1 Min Read
Juma Jux na Priscilla Ojo

Mwanamuziki wa Tanzania Juma Jux amesema kwamba anafanya mipango ya kufunga ndoa na mpenzi wake wa Nigeria Priscilla Ojo mwaka ujao wa 2025.

Haya yalifahamika kupitia video iliyochapishwa mitandaoni ya mawasiliano ya video kati ya Juma Jux na rafiki ya Ojo kwa jina Chioma.

Ojo alikuwa nyuma ya Chioma wakati mazungumzo hayo yalikuwa yakiendelea huku akichekacheka.

Jux ambaye aliwahi kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Vanessa Mdee, alimtambulisha Ojo mitandaoni mwezi septemba ambapo alisafiri hadi Nigeria kumwona.

Awali wengi walidhania kwamba uhusiano wao haukuwa wa kweli na kwamba walikuwa tu wanashirikiana kwenye video ya muziki lakini umetokea kuwa wa kweli.

Mamake Priscilla ambaye ni mwigizaji maarufu nchini Nigeria kwa jina Iyabo Ojo alitangaza uhusiano wa wawili hao kwenye mitandao ya kijamii Septemba 2, 2024.

Alidhihirisha kwamba anawaunga mkono huku akimrejelea mwanawe kuwa mke wa mtu.

Juma Jux aliingia kwenye mahusiano na Priscilla baada ya uhusiano wake na Karen Bujulu wa Tanzania kuvunjika.

Inaaminika kwamba video ya Jux akimbusu mwanamitindo wa Kenya Huddah Monroe ilikuwa chanzo kikuu cha kuharibika kwa uhusiano kati ya wawili hao.

Website |  + posts
Share This Article