JSC: Jihadhari dhidi ya walaghai wenye nia ya kuwapora pesa

Martin Mwanje
1 Min Read

Tume ya Huduma za Mahakama, JSC imetoa wito kwa Wakenya kuchukua tahadhari dhidi ya watu inaosema wanajisingizia kuwa wafanyakazi wa tume hiyo na wanaowahadaa kuwapatia fedha kwa ahadi kwamba watawasaidia kupata ajira katika idara ya mahakama.

JSC inasema inatoa ajira kwa usawa na inawateua waliotuma maombi kupitia mchakato wenye usawa na uwazi kutoka kwa wagombea mbalimbali wanaostahiki.

“Walaghai hao kupitia kupiga simu au kutuma arafa wanaitisha fedha ili kupata kazi katika nyadhifa zilizotangazwa siku chache zilizopita,” ilisema JSC katika taarifa.

Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome pia imewashauri waliotuma maombi dhidi ya kutumia njia za mkato ikisema maombi ya wale watakaopatikana yatatupiliwa mbali.

Ili kupata taarifa halali kutoka JSC, Wakenya wametakiwa kutembelea mitandao rasmi ya kijamii ya tume hiyo.

JSC imetangaza nyadhifa mbalimbali katika idara ya mahakama ikiwa ni pamoja na zile za majaji wa Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu.

 

 

Share This Article