Mwigizaji mkongwe wa Nollywood nchini Nigeria Joke Silva amekanusha taarifa zilizosambazwa mitandaoni kuhusu kifo cha mume wake.
Akizingumza kwenye mahojiano, Silva alisema mume wake kwa jina Olu Jacobs ambaye pia ni mwigizaji mkongwe bado yuko hai hata ingawa anaugua.
Hii ni mara ya pili taarifa kama hizo zinasambazwa mitandaoni. Zamu hii ilibidi familia ya mzee huyo ichapishe video inayomwonyesha akinyolewa nyumbani kwake.
Agosti 2022, mitandao ilijaa taarifa sawia za kutangaza kifo cha mwigizaji huo ambazo Joke Silva alilazimika kuzima huku akitishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wasambazaji wa taarifa hizo za uwongo.
Olu Jacobs ambaye ameigiza kwenye filamu nyingi za Nigeria alichukua mapumziko kutoka kwa fani hiyo kutokana na matatizo ya kiafya
ambayo yanamsibu hadi sasa.
Anaugua ugonjwa wa Dementia ambao unadhihirika kwa dalili kama vile kutokumbuka, kupoteza uwezo wa kufikiria na kupoteza uwezo wa kufanya maamuzi hali ambay hufanya iwe vigumu kwa mtu kutekeleza majukumu ya kila siku.
Mzee huyo ana tajriba ya miaka karibu 40 katika uigizaji na wengi humchukulia kuwa kiungo muhimu kati ya waigizaji wa jadi wa Nollywood na wa sasa.