Shule za wavulana za St.Joseph (JOBO) na Musingu kutoka eneo la Bonde la Ufa na Magharibi mtawalia, zitakabana koo hapo kesho katika nusu fainali ya michuano ya Kitaifa ya muhula wa pili baina ya shule za upili (KSSSA) inayoendelea mjini Kisii.
Mchuano huu umebainika baada ya JOBO kushinda mechi yake ya kutegemewa na ya mwisho leo mchana dhidi ya St. Aggrey ya eneo la Pwani bao sita kwa nunge na kuebuka wa pili kwa alama sita katika kundi B nyuma ya Highway ya eneo la Nairobi iliyo na lama saba.
Musingu nayo ilifuzu hapo jana kufuatia ushindi wa pili dhidhi ya Kirangari ya eneo la Kati.Vile vile walipata ushindi wa tatu hii leo kwa kuwalaza wenyeji Koderobaro bao moja kwa sufuri na kuongoza kundi hilo kwa alama tisa licha mashabiki kuingia uwanjani na kusababisha mchezo huo kusimamishwa kwa muda.
Uwepo wa Musingu katika hatua hii kwa muda wa miaka ishirini, unafutia ujio wa miaka tano iliyopita wa mwalimu na kocha wa zamani wa shule ya wavulana ya Kakamega ( Green Commandoes) Brendan Mwinamo.
Nusu fainali ya pili ni baina ya viongozi wa kundi B Highway ya Nairobi na namabari mbili wa kundi A Kirangari.
Kwenye mchuano huu, Highway inao uwezo mkubwa wa kunawiri kwani imeshinda mechi mbili dhidi ya JOBO na Tabaka ya eneo la Mashariki ya Kati na kutoka sare dhidi ya St. Aggrey ya Pwani.
Pia inajivunia ufundi wa kocha wake Beldine Ademba, aliye pia mkufunzi wa timu ya taifa ya wanadada (Harambee Starlets) na Vipusa wa Kenya Police.
Mwaka 2022, Beldine aliiongoza shule hiyo kumaliza wa pili dhidi ya Ebwali ya Magharibi walioshinda tuzo hilo mjini Nakuru. Kufuatia matokeo hayo, walifuzu Kwa mashindano ya Afrika Mashariki (FEASSSA) ambapo pia walinawiri.