Shule za St.Joseph Boys (JOBO) kutoka eneo la bonde la ufa imenyakua taji la kitaifa la soka baina ya shule za upili baada ya kuilaza Musingu bao moja kwa nunge kwenye fainali ya mashindano ya kitaifa baina ya shule za upili ambayo yameisha leo Jumamosi.
Ngarambe hiyo yenye halaiki ya mashabiki na ambayo ilisakatwa katika uga wa Mumias Complex katika kaunti ya Kakamega, ilihudhuriwa na viongozi wengi akiwemo gavana wa kaunti ya kakamega Fernandes Barasa.
Kwa wengi, ushindi huu ulikuwa wa kulipiza kisasi cha mwaka jana ambapo Musingu iliicharaza JOBO kwenye nusu fainali kupitia matuta.
Taji hilo ni la kwanza kwa shule hiyo ambayo iliaanzisha mradi huo wa soka miaka chache iliyopita chini ya uongozi wa mwalimu mkuu mwenye uzoefu wa kandanda ya shule za upili – Cosmas Nabungolo. Awali mwalimu huyo aliiongoza shule ya St. Antony kushinda taji hilo mara kadhaa.
Kwa Musingu, Hii ni mara ya pili mtawalia kupoteza katika fainay kwani pia mwaka jana walilazwa na Highway kwa njia ya matuta. Mara ya pekee ya shule hiyo kunyakua tuzo hilo ulikuwa mwaka wa 1984.
Katika upande wa vidosho, wenyeji Butere waliwapiku wenyeji wenzao Madira kwa bao moja kwa bila na kuebuka mabingwa kwa mara ya tatu mtawalia.
Kwenye voliboli, wavulana wa Cheptil waliwazaba Malava nao vipusa wa Kwanzanze wakawalemea wa Kesogon.
Pia kuliandaliwa raga ya wachezaji saba kila upande ambapo St.Peters walivuna ushindi wa alama 14 kwa12 za Koyonzo nao Warembo wa kinale wakawalaza wenzao wa St.Joseph.
Na kama ilivyo kawaida yao, wasichana wa Buruburu walituzwa taji la mchezo wa vikapu vya wachezaji watatu kila upande sawia na wavulana wa Sigalame.
Washindi wengine wa mwaka huu ni wanamwali wa Oyugi Ongango waliowazidi St.Joseph katika mchezo wa Pete.
Washindi hawa na wale wa nafasi ya pili hadi nne, watawakilisha taifa kwenye mashindano ya Afrika Mashariki ( FEASSSA) baina ya shule za upili yatakayoandaliwa hapa nchini mjini Kakamega baada ya juma moja lijalo.
Kuandaliwa kwa mashindano hayo katika kaunti ya Kakamega kunatoa nafasi moja zaidi kwa kila kitengo kwa shule za Kaunti hiyo.
Kwa mujibu wa waandalizi wa kipute hicho kwa ushirikiano na serikali ya kaunti hiyo , shule zilizomaliza za pili katika mashindano ya kaunti hiyo zitashiriki.