Mshindi wa shindano la ulimbwende la Miss Grand International mwaka 2026, Jihan Dimack, amewashukuru Watanzania kwa upendo, mshikamano na kumuunga mkono katika safari yake ya kutwaa taji hilo la kimataifa.
Jihan alitoa shukrani hizo jana Oktoba 17, 2026, jijini Dar es Salaam, katika hafla maalum ya mapokezi na kusherehekea ushindi wake, akieleza furaha yake kwa waliojitokeza kuungana naye.
Katika hotuba yake, mrembo huyo aliwashukuru raia wa Tanzania kwa kuwa sehemu muhimu ya safari yake ya mafanikio, kwa kumpigia kura kwa wingi, huku akimshukuru Mungu kwa kuwawezesha kusherehekea ushindi huo pamoja.
Jihan aliwasili nchini Tanzania jana, akitokea jijini Bangkok, nchini Thailand, baada ya kutwaa taji la Miss Grand International mwaka 2026. Alipokelewa na umati mkubwa wa watu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Baada ya mapokezi, msafara wake ulipita katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo, huku wananchi wakijitokeza kusherehekea mafanikio yake.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa aliyehudhuria hafla hiyo, alisema ushindi huo ni ujumbe kwa dunia kwamba Tanzania ni nchi ya amani, umoja na mshikamano.
Msigwa aliongeza kuwa mafanikio ya Jihan yamewaunganisha Watanzania na kuwafanya kujivunia nchi yao kwa pamoja.
Ushindi wa Jihan unaweka Tanzania katika ramani ya mashindano ya kimataifa ya urembo.