Nameless afuta matamasha kisa matatizo ya kiafya

Alifaa kutumbuiza ndani ya Wave XO mjini Nakuru Ijumaa, kwenye Loop Safari Gravel Series mjini Nanyuki na Kettle House jijini Nairobi Jumamosi, Oktoba 17.

Marion Bosire
1 Min Read

Msanii maarufu wa muziki nchini Kenya David Mathenge, maarufu kama Nameless, alilazimika kufuta maonyesho matatu yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Nairobi, Nakuru na Nanyuki wikendi hii baada ya kuugua.

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, Oktoba 16, 2026, mwimbaji huyo aliwaomba radhi mashabiki waliouwa wakitarajia burudani kutoka kwake na waandaaji wa hafla hizo, akisema hali yake ya kiafya haikumruhusu kutumbuiza.

Nameless alifichua kuwa amekuwa akisumbuliwa na homa kali, udhaifu mkubwa wa mwili, kikohozi na kupoteza sauti kwa siku kadhaa. Alisema licha ya juhudi za kupona kabla ya wikendi, bado hakuwa na uwezo wa kupanda jukwaani.

Maonyesho yaliyoathiriwa ni ya eneo la burudani la Wave XO mjini Nakuru Ijumaa, onyesho la Loop Safari Series mjini Nanyuki na katika eneo la burudani la Kettle House jijini Nairobi Jumamosi, Oktoba 17.

Msanii huyo alieleza kusikitishwa na kukosa maonyesho hayo, akiwahakikishia mashabiki kuwa anathamini uungwaji mkono wao na ana matumaini ya kufidia maonyesho yaliyofutwa.

Aliongeza kuwa tarehe mpya za maonyesho hayo zitatangazwa baadaye.

Nameless alipata umaarufu mwanzo wa miaka ya 2000 na anasalia kuwa miongoni mwa wanamuziki mashuhuri nchini Kenya ambao wana ushawishi mkubwa, akiwa na zaidi ya miongo miwili katika tasnia ya muziki.

Share This Article