Azziad Nasenya aomboleza kifo cha babu yake mpendwa

Ameelezea jinsi anavyopambana kukubali maisha bila uwepo wake.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwigizaji, mtayarishaji wa maudhui mitandaoni na mtangazaji maarufu nchini Kenya Azziad Nasenya, anaomboleza kifo cha babu yake mpendwa, Shaban Caxton Wafula, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 77.

Azziad alitoa habari hizo za kuhuzunisha kwa wafuasi wake kupitia mitandao ya kijamii, akichapisha mkusanyiko wa picha za zamani na za hivi karibuni zinazoonyesha uhusiano wa karibu waliokuwa nao nyumbani kwa familia yao mjini Mumias.

Katika ujumbe wa kumuenzi mzee huyo, mtangazaji huyo wa redio na mshawishi wa mitandaoni alimwelezea marehemu kama rafiki yake mkubwa wa muda mrefu zaidi, huku akieleza jinsi anavyopambana kukubali maisha bila uwepo wake.

Baada ya kutangaza kifo hicho, mashabiki, watayarishaji wenzake wa maudhui na watu mbalimbali maarufu walijitokeza katika sehemu ya maoni kwenye machapisho yake kutoa rambirambi na faraja kwa familia.

Shix Kapienga, Ajib Gathoni, Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya na Ali Manzu ni kati ya watu maarufu waliompa pole Azziad Nasenya.

Share This Article