Wanajeshi wa Israel walitekeleza mashambulizi katika hospitali ya Kamal Adwan ambayo iko katika eneo la kaskazini mwa Gaza.
Wamevamia hospitali hiyo mara kadhaa tangu walipozindua mashambulizi ya Gaza Kaskazini Oktoba 6.
Wahudumu wawili wa hospitali hiyo walifariki kwenye shambulizi huku wengine 12 wakiachwa na majeraha akiwemo mkurugenzi Abu Safiya.
Kituo cha habari cha Palestina kilichapisha picha za daktari Hussam Abu Safia akiwa kwenye machela huku wahudumu wakifunga mguu wake uliokuwa umejeruhiwa.
Alitaja kujeruhiwa kwake kuwa heshima kubwa.
Mtambo wa kuzalisha umeme hospitalini humo na mifumo ya kusambaza hewa ya Oxygen na maji viliharibiwa kabisa.
Kundi la Hezbollah kutoka Lebanon nalo limedai kushambulia wanajeshi wa Israel kwa kutumia makombora katika eneo la Kfar Blum.
Lilikiri kutekeleza mashambulizi 34 katika maeneo mbali mbali ya Israel Kaskazini mwa Israeli na Kusini mwa Lebanon Jumamosi, likiwemo shambulizi la kombora katika mji wa Al-Bayyaada nchini Lebanon.
Mashambulizi hayo yalisababisha vifo kadhaa na majeruhi huku Israel ikishambulia maeneo mbali mbali ya Lebanon.
Watu wapatao 20 waliuawa huku 66 wakiachwa na majeraha kufuatia mashambulizi ya Israel katikati mwa Beirut, na kuhujumu mipango ya kusitisha vita kati ya Hezbollah na Israel.