Jengo labomoka Shauri Moyo, shughuli za utafutaji na uokozi zaendelea

Martin Mwanje
1 Min Read

Jengo moja limebomoka katika eneo la Blue Estate katika mtaa wa Shauri Moyo, kaunti ndogo ya Kamukunji katika kaunti ya Nairobi. 

Hii ilitokana na jaribio la kulibomoa jengo hilo mapema leo Jumatatu.

Jengo hilo ni miongoni mwa yale yaliyojengwa karibu na mto Nairobi ambayo yamepangwa kubomolewa chini ya mpango unaoendelea wa usafishaji mto huo.

Kwenye taarifa, Wizara ya Usalama wa Ndani inasema watu kadhaa huenda wamenaswa kwenye jengo hilo.

Vikosi vya Ulinzi nchini, KDF, Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS, maafisa wa utawala wa serikali kuu na Shirika la Msalaba Mwekundu ni miongoni mwa waliotumwa eneo la tukio kusaidia katika shughuli za utafutaji na uokozi.

Hadi kufikia sasa, watu wawili wameokolewa kutoka kwenye ukuta ulioanguka. Mmoja wa watu hao alipata majeraha madogo na alikimbizwa hospitalini kwa matibabu ilhali mwingine yu buheri wa afya.

Watu wametakiwa kutokaribia eneo hilo ili kuruhusu shughuli za utafutaji na uokozi kuendelea bila vizuizi.

Share This Article