Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya kilomita 10 Agnes Jebet Ng’etich, na mshindi wa nishani ya fedha ya dunia katika mita 10,000 Daniel Ebenyo Simiu, ndio mabingwa wa mbio za kilomita 10 katika makala ya 4 ya mashindano ya Absa Sirikwa Classic World Cross Country Tour, yaliyoandaliwa leo eneo la Lobo, Kapseret, jijini Eldoret.
Jebet, ambaye pia ni mwanariadha mwenye kasi zaidi katika mbio za nusu marathoni, aliongoza kutoka mwanzo hadi mwisho na kunyakua nishani ya dhahabu kwa kutumia muda wa dakika 32 na sekunde 42, sekunde 10 mbele ya Janeth Chepngetich, aliyetwaa fedha huku Mirriam Chebet akiridhia shaba kwa dakika 34 na sekunde 9.
Simiu Ebenyo alitawala mbio za wanaume na kutetea taji yake kwa kutumia dakika 29 na sekunde 57, akifuatwa na Gideon Ronoh, aliyeziparakasa kwa dakika 30 na sekunde saba kushinda medali ya fedha huku Nicholas Kipkorir, akinyakua shaba kwa dakika 30 na sekunde 15.
Kevin Kiprop na Cynthia Chepkurui walishinda mbio za kilomita 8 na kilomita 6 kwa wavulana na wasichana chini ya umri wa miaka 20 mtawalia.
Waliokuwa mabingwa wa dunia kwa chipukizi walio chini ya umri wa miaka 20, Reynold Cheruiyot na Purity Chepkurui, walitawazwa mabingwa wa mbio za kilomita 2 kwa wanaume na wanawake katika usanjari huo.
Washindi wa medali za dhahabu katika mbio za kilomita 10 walituzwa shilingi laki saba na elfu 80, shilingi 650,000 kwa washindi wa nishani za fedha, nao washindi wa shaba wakanyakua shilingi 520,000.
Zaidi ya wanariadha elfu moja kutoka mataifa 40 walishiriki makala ya mwaka huu kando na mbio za watoto.