Makubaliano muhimu ya kushirikiana katika matumizi ya malisho yaliyosalia yamesainiwa kati ya jamii tatu za wafugaji – Warendille kutoka kaunti ya Marsabit, Wasamburu kutoka kaunti ya Samburu, na Waborana kutoka kaunti ya Isiolo – ili kutumia kwa pamoja rasilimali zilizobaki za maji na malisho kufuatia ukame mkali uliosababisha mifugo zaidi ya 10,000 kuingia katika eneo la Kom Triangle, kandokando ya Mto Ewaso Ng’iro, mahali ambapo kaunti hizo tatu hukutana.
Makubaliano hayo yamekuja wakati ambapo kuna hofu inayoongezeka kuhusu wizi wa mifugo na ukosefu wa usalama, huku ripoti zikielezea kuwa vijana waliojihami kwa silaha haramu wamekuwa wakiwasindikiza wafugaji na mifugo wao, na wengine kuripotiwa kusimamisha magari kwa njia isiyo halali katika barabara ya Kom–Merti.
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo, Naibu Kamishna wa kaunti ya Samburu Mashariki Stanley Langat alisema kuwa makubaliano hayo yanalenga kudhibiti uhamaji wa mifugo katika maeneo ya malisho yanayotumiwa pamoja ili kuzuia mapigano na kuhakikisha sheria na utulivu vinazingatiwa.
Hati ya makubaliano hayo ilisainiwa na makamishna wa kaunti ndogo tatu pamoja na wawakilishi wa jamii husika, na itatekelezwa kwa kipindi chote cha ukame huu, ambao wataalamu wa hali ya hewa wameonya kuwa huenda ukaendelea kwa muda mrefu kuliko kawaida.
Langat aliwahakikishia wakazi kuwa serikali inafuatilia hali hiyo kwa karibu na itatuma maafisa wa utawala katika maeneo ya malisho ili kuhakikisha wafugaji wanazingatia masharti ya makubaliano hayo.
Mwakilishi wa wadi ya Waso Kelvin Lemantaan alipongeza hatua hiyo, akieleza kuwa machifu watahitajika kuwasindikiza wafugaji kuhakikisha masharti ya makubaliano yanatekelezwa. Pia alizihimiza jamii kuhakikisha mifugo iliyoibwa kabla ya makubaliano hayo inarudishwa kwa wamiliki wake, na kuandaa mikakati ya kuwaondoa watoto wa shule katika maeneo ya malisho ili warejelee masomo.
Saiyana Lempara, Meneja wa Mpango wa Malisho unaotekelezwa na Baraza la Maendeleo ya Kaunti za Mpakani (FCDC), aliwataka wadau wote kushirikiana kuandaa mpango madhubuti wa kuwafikishia wafugaji walioko maeneo ya malisho masharti ya makubaliano hayo kwa njia iliyo wazi na yenye kueleweka, ili kuhakikisha yanazingatiwa hadi hali ya ukame itakapopungua.
Wakati huohuo, Naibu Kamishna wa kaunti Ndogo ya Laisamis, Kepha Marube, aliwaagiza manaibu machifu kufuatilia wafugaji wanapohama ili kuhakikisha uwajibikaji katika msimu mzima wa ukame. Pia amewasihi wazee wa jamii kuhimiza watoto na vijana kuthamini elimu kama njia ya muda mrefu ya kuimarisha usalama wa jamii.